Kikosi kazi chawasilisha ripoti yake kwa Rais

0
274

Kikosi Kazi cha Kuratibu Maoni ya Wadau wa Demokrasia ya vyama vingi vya siasa , leo kimewasilisha ripoti yake kwa Rais Samia Suluhu Hassan.

Hafla ya kukabidhi ripoti hiyo imefanyika Ikulu mkoani Dar es Salaam, baada ya kikosi hicho kufanya kazi hiyo kwa takribani miezi kumi.

Miongoni mwa mapendekezo ya kikosi kazi hicho ni mikutano vya hadhara ya vyama vya siasa iruhusiwe na ile mikutano ya ndani ya vyama vya siasa nayo ifanyike bila vikwazo.

Mapendekezo mengine yaliyowasilishwa na Mwenyekiti wa kikosi kazi hicho Profesa Rwekaza Mukandala ni matokeo ya uchaguzi wa Urais yahojiwe kwenye Mahakama ya Juu pindi itakapoanzishwa.

Pia kikosi kazi hicho kimependekeza Tume ya Taifa ya Uchaguzi isikubali kufuata maelekezo ya mtu yeyote, kikundi chochote ama chama chochote na iweze kuhojiwa na Mahakama ya Juu.

Mapendekezo mengine ni kufanyiwa maboresho kwa sheria ya vyama vya siasa na mfumo wa kugawa ruzuku kwa vyama vya siasa nao ufanyiwe maboresho.

Kuhusu katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kikosi kazi hicho kimependekeza kufanyika kwa mambo kadhaa ikiwa ni pamoja na mchakato wa kupata katiba hiyo uendelee kwa kufuata michakato mbalimbali ikiwa ni pamoja na kufanyika kwa mjadala wa kitaifa kwenye mambo ya msingi.

Kikosi Kazi cha Kuratibu Maoni ya Wadau wa Demokrasia ya vyama vingi vya siasa, katika kutekeleza majukuku yake kimepata maoni ya watu mbalimbali akiwemo Rais Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Mwinyi.