Serikali kufanyia kazi mapendekezo ya kikosi kazi

0
257

Rais Samia Suluhu Hassan amesema, serikali itayafanyia kazi mapendekezo yote yaliyotolewa na Kikosi Kazi cha Kuratibu Maoni ya Wadau wa Demokrasia ya Vyama vingi vya siasa.

Rais Samia Suluhu Hassan ameyasema hayo Ikulu mkoani Dar es Salaam, alipokuwa akipokea ripoti ya kikosi kazi hicho baada ya kukamilisha kazi yake.

Amesema mapendekezo yanayoonekana ni mepesi yaliyotolewa na kikosi kazi hicho yatafanyiwa kazi haraka iwezekqnavyo na yale yanayoonekana kuwa ni magumu yatachambuliwa taratibu.

Hata hivyo Rais Samia Suluhu Hassan amesema mapendekezo ya kikosi kazi hicho si amri kwa serikali kuwa ni lazima yatekelezwe, bali yatachambuliwa na kuona kipi kitafanyiwa kazi.

Wakati serikali ikienda kuchambua mapendekezo hayo, Rais Samia Suluhu Hassan amevitaka vyama vya siasa nchini visifanye kazi ya kuikosoa tu serikali, bali navyo vijitazame vinajiendesha vipi.

Kikosi Kazi hicho cha Kuratibu Maoni ya Wadau wa Demokrasia ya Vyama vingi vya siasa kilikuwa kikiongozwa na Profesa Rwekaza Mukandala na kimefanya kazi yake kwa muda wa miezi kumi.