Masanja aelekeza watumishi wa wizara wasio waadilifu wawajibishwe

0
275

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja amewaagiza Wakuu wa Wilaya nchini kuwawajibisha watumishi wa Wizara ya Maliasili na Utalii wasio waadilifu katika kusimamia maeneo ya hifadhi.

Ameyasema hayo leo Oktoba 19, 2022 wakati wa Kikao cha Kamati ya Mawaziri wa Kisekta ya kutatua migogoro ya ardhi katika vijiji 975 nchini, kilichofanyika katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza.

“Niwaombe kama kisababishi cha uvamizi katika maeneo ya hifadhi ni watumishi wa Wizara ya Maliasili na Utalii Mkuu wa Wilaya una nafasi ya kuwawajibisha kwa kushirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii” amesema.

Amefafanua kuwa kama watayasimamia vizuri maeneo yaliyohifadhiwa wananchi hawataendelea kuyavamia kwa sababu maeneo mengi yamevamiwa kutokana na viongozi wa eneo husika kuyaachia bila usimamizi wowote, na kwamba uvamizi huo unaathiri utekelezaji wa majukumu ya wizara nyingine.

Aidha, amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuruhusu idadi ya vijiji 920 nchini kuachiwa kwa wananchi kati ya vijiji 975 vilivyokuwa na migogoro ya ardhi ambapo vijiji 55 pekee vinaendelea kupatiwa ufumbuzi.

Katika jiji la Mwanza jumla ya vijiji 48 vina migogoro ya ardhi ambapo kati ya hivyo vijiji 14 viko katika Hifadhi ya Pori la Sayaka lililopo Wilayani Magu.
Vijiji hivyo vitaandaliwa mpango wa matumizi bora ya ardhi ili kuwafanya wananchi kuwa wahifadhi na walinzi wa hifadhi hiyo.