Timu ya Taifa ya Wanawake chini ya Miaka 17 (Serengeti Girls), inatarajia kucheza na Colombia katika robo fainali baada ya kuandika historia kwa mara kwanza kufuzu hatua ya Robo Fainali ya Kombe la Dunia baada ya kuitoa timu ya Canada.
Mechi ya Robo Fainali baina ya Tanzania (Serengeti Girls) na Colombia itachezwa Oktoba 22, jijini Goa India.
Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Pauline Gekul ameishukuru Serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha timu hiyo ya Serengeti kuanzia kuweka Kambi ya kutosha katika Mji wa Southampton nchini Uingereza ambapo ilifanya maandalizi mazuri ambayo yameifikisha hapo timu hiyo.
Kwa upande wa Kocha Bakari Shime, amesema Wasichana wamefanya vizuri baada ya kufuata maelekezo aliyowapatia pamoja na kurekebisha makosa waliyoyaona katika mechi zao mbili za kwanza, huku akisema Wasichana hao siku zote wana ari ya ushindi na wamekua na utulivu kiakili pamoja na nidhamu ya hali ya juu.