Waziri Mkuu aagiza milango ya hospitali ing’olewe

0
236

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amekagua ujenzi wa hospitali ya wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma na kueleza kutoridhishwa na maendeleo ya ujenzi huo.

Akikagua ujenzi huo Waziri Mkuu amejionea baadhi ya milango imepishana urefu licha ya kuwa inapaswa ikutane ili kitasa kiweze kufunga, huku mingine ikiwa inagoma kufunga, inarudi nyuma na kubakia wazi.

Akizungumza mara baada ya kuona hali hiyo Waziri Mkuu Majaliwa amesema serikali haiwezi kukaa kimya wakati tayari imetoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa hospitali hiyo ya wilaya ya Namtumbo, huku baadhi ya watumishi wakifanya vitendo vya hovyo.

“Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ameleta shilingi bilioni saba za ujenzi wa hospitali hii, fedha hizi za ujenzi ni lazima wananchi waone thamani ya fedha zao. Siwezi kukubaliana na utendaji wa hovyo fedha ziko hapa tangu Aprili, ni kwa nini hadi sasa majengo yapo kwenye lenta?.” amehoji Waziri Mkuu Majaliwa na kuongeza kuwa

“Nimekagua ujenzi wa hospitali ya wilaya lakini sijaridhishwa na hali ya ujenzi, nimeagiza milango yenye hitilafu yote ing’olewe na iwekwe yenye hadhi ya hospitali ya wilaya. Iweje imeacha nafasi juu hadi vidole vinapita?, mtu akifunga mlango wewe uliyeko nje unaona ndani. Hii haikubaliki, RC simamieni milango hiyo itolewe na ije yenye hadhi.”