Bomu lajeruhi watoto Tabora

0
122

Watoto wawili wa kijiji cha Kabila katika manispaa ya Tabora wamejeruhiwa sehemu mbalimbali za miili yao baada ya kulipukiwa na kitu kinachodhaniwa kuwa ni bomu walilolikata kwa kutumia panga.

Kamanda wa polisi wa mkoa wa Tabora, Richard Abwao amewataja watoto hao waliojeruhiwa kuwa ni Kikombe Kishagembe (17) na Said Dulu (10) ambao walilikata bomu hilo ili kutaka kufahamu ni kitu gani.

Amesema tukio hilo limetokea wakati watoto hao wakichunga ng’ombe ndani ya hifadhi ya Taifa ya Igombe na kuokota kitu ambacho walitaka kufahamu kilikuwa nini.

Kamanda Abwao amesema watoto hao walichukua kitu hicho hadi nyumbani na kisha kutaka kufahamu kilikuwa na nini ndani yake, hivyo walichukua panga na kukata, ndipo mlipuko ukatokea na kuwajeruhi.

Amesema watoto hao wamejeruhiwa sehemu kadhaa za miili yao ikiwa ni pamoja na mikononi, miguuni na mapajani.

Kamanda Abwao ameeleza kuwa uchunguzi wa awali umebaini kuwa kitu hicho ni bomu aina ya Stick Hand Grunet na kwamba wanaendelea na uchunguzi wa tukio hilo kwa kushirikiana na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).

Amesema majeruhi hao wanapatiwa matibabu katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Tabora -Kitete.