Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) Dkt. William Kisinza amesema, wagonjwa 9,545 nchini wamefanyiwa upasuaji wa mabusha.
Dkt. Kisinza amesema kati ya wagonjwa hao, 3,115 ni kutoka mkoa wa Lindi.
Amesema hayo mkoani Lindi wakati wa kongamano la uwasilishaji wa matokeo ya utafiti wa ugonjwa wa mabusha na matende uliofanywa na NIMR kupitia mradi wa kupambana na vikwazo vya kutokomeza matende na mabusha nchini.
Dkt. Kisinza
amesema kati ya mwaka 1998 na 2004, NIMR ilifanya utafiti katika mkoa wa Lindi na kubaini kiwango cha maambukizi ya matende na mabusha kati ya asilimia 47 na 60 katika halmashauri za Nachingwea, Liwale na Mtama.
Utafiti huo ulipelekea kuanzishwa kwa Mpango wa Taifa wa kutokomeza ugonjwa wa matende kwa kutumia afua ya ugawaji wa dawa za kingatiba za Albendanzole na Ivermectin katika ngazi ya jamii.
Dkt. Kisinzo amesema kutoka na juhudi hizo, maambukizi ya magonjwa hayo yamepungua na kufikia kiwango cha kati ya asilimia 2.3 na 6.2 katika halmashauri za Nachingwea, Liwale na Ruangwa.