Tanzania na Kenya kukomesha vitendo vya ugaidi

0
568

Tanzania na Kenya zimekubaliana kushirikiana kukabiliana na vitendo vya ugaidi na usafirishaji wa binadamu, ili kuhakikisha nchi zote zinakuwa salama.

Rais wa Kenya, Dkt. William Ruto amesema hayo Ikulu, Dar es Salaam alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu masuala waliyozungumza alipokutana na Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.

Amesema kuwa usalama wa Kenya na Tanzania unategemeana, hivyo ushirikiano huo ambao pia utajumuisha ushirikiano wa mawasiliano vitawezesha kukabiliana na uhalifu unaochafua taswira za nchi zote mbili.

Mapema akizungumzia vitendo hivyo Rais Samia Suluhu Hassan alisema kuwa licha ya kwamba Tanzania na Kenya hazihusiki na vitendo vya usafirishaji wa binadamu, lakini pindi wanapokamata watu kwa vitendo hivyo taarifa zinazokwenda duniani zinaathiri nchi hizo, hivyo ni vyema wakadhibiti.