Watano wasimamishwa kazi Mbulu

0
110

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Innocent Bashungwa amewasimamisha kazi maafisa watano wa halmashauri ya wilaya ya Mbulu mkoani Manyara, ili kupisha uchunguzi wa tuhuma za kusababisha hasara na matumizi mabaya ya madaraka.

Maafisa hao ni kaimu mkuu wa kitengo cha manunuzi Juma Mavumo, aliyekuwa kaimu mweka hazina Ramadhani Mwakamyanda, Mweka hazina wa sasa Respicius Kagaruki, mkuu wa kitengo cha TEHAMA Nyanda Msirikale na mhasibu wa mapato David Assey.

Waziri Bashungwa amechukua hatua hiyo wakati akifanya majumuisho ya ziara yake ya kikazi iliyokuwa na lengo la kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa kwenye halmashauri ya wilaya ya Mbulu, halmashauri ya wilaya ya Hanang’ na halmashauri ya Mji Mbulu mkoani Manyara.

Julai 12 mwaka huu aliyekuwa anakaimu ofisi ya Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya Mbulu, David Assey anadaiwa kuandika barua kwa kampuni binafsi na kukopa shilingi milioni 6.7 kwa aijli ya matumizi ya ofisi na kuelekeza fedha hiyo kuwekwa kwenye akaunti yake binafsi.