DRC kuunganishwa na Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano

0
192

Serikali kupitia wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imewahakikishia wabunifu wa TEHAMA fursa ya kutangaza bidhaa zao kupitia kongamano la fursa la mashirikiano baina ya Tanzania na Jamhuri ya
Kidemokrasi ya Congo (DRC) kwenye sekta ya mawasiliano.

Kauli hiyo imetolewa mkoani Dar es Salaam na
waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari kuhusu kongamano hilo linalotarajiwa kufanyika DRC.

Amesema kupitia kongamano hilo la fursa ya mashirikiano kwenye sekta ya mawasiliano,
mambo mabalimbali yatajadiliwa ukiwemo mpango wa kuiunganisha DRC na Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano ili kurahisisha huduma za mawasiliano kwa wafanyabishara na wabunifu wa TEHAMA.

Aidha Waziri Nape amebainisha kuwa kongamano hilo litazisaidia kampuni changa kupata fursa ya kutambulika kimataifa, hivyo amewasisitiza wabunifu kushiriki kwa wingi.

Kwa upande wake kaimu Balozi wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo nchini Kanupangi Yamba Yamba Gilbert, ameahidi ushirikiano katika kufanikisha kongamano hilo muhimu kwa ustawi wa pande hizo mbili.

Takribani kampuni hamsini za ubunifu za huduma ya TEHAMA zinatarajiwa kushiriki katika kongamano hilo litakalofanyika Oktoba 18 na 19 mwaka huu huko Lubumbashi.