FRELIMO yajinasibu kufanya makubwa

0
148

Mwenyekiti wa chama tawala nchini Msumbiji cha Mozambican Liberation Front (FRELIMO) Rais Filipe Nyusi amesema, chama hicho kitahakikisha wananchi wanafikiwa na huduma zote muhimu.

Akihutumia kongamano la 12 la chama cha FRELIMO Rais Nyusi amesema, Msumbiji ina rasilimali nyingi hivyo ni lazima zitumike vizuri katika kuwafikishia huduma mbalimbali wananchi.

Amesema jitihada za kuwafikishia wananchi huduma mbalimbali zimekuwa zikikwamishwa na mambo kadhaa ikiwa ni pamoja na vita miaka ya nyuma na mashambulio ambayo yamekuwa yakitekelezwa na vikundi vya kigaidi.

Hata hivyo amesema serikali ya Msumbiji chini ya chama cha FRELIMO inaendelea kukabiliana na vikwazo hivyo, ili kuhakikisha huduma hizo zinawafikia wananchi.

Lengo la kongamano hilo la 12 la chama cha FRELIMO ni kuweka mikakati imara kwa ajili ya kukiendeleza chama hicho pamoja kuisimamia serikali.

Mada mbalimbali zinajadiliwa katika kongamano hilo ikiwa ni pamoja na kuimarisha umoja wa kitaifa, mapambano dhidi ya ugaidi na namna ya kupata ushindi katika chaguzi zijazo.

Kongamano hilo linashirikisha wageni mbalimbali akiwemo Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania ambaye yupo nchini Msumbiji kwa ziara ya kiserikali ya siku tatu.

Kongamano hilo la 12 la chama cha FRELIMO linafanyika wakati chama hicho kikiwa kimetimiza miaka 60 tangu kuasisiwa kwake.

Chama hicho kiliasisiwa June 25 mwaka 1962 mkoani Dar es Salaam na Hayati Eduardo Mondlane na Hayati Samora Machel.