Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango ametoa wito kwa mataifa mbalimbali duniani kuuchangia mfuko wa kimataifa wa kupambana na Ukimwi, Kifua Kikuu na Malaria (Global Fund).
Amesema hatua hiyo itausaidia mfuko huo kufikia lengo la kukusanya dola bilioni 18 za kimarekani, zitakazotumika kutokomeza magonjwa hayo duniani kwa kipindi cha miaka mitatu ijayo.
Dkt. Mpango ametoa kauli hiyo wakati akihutubia mkutano wa saba wa kuuwezesha mfuko huo wa kimataifa wa kupambana na Ukimwi, Kifua Kikuu na Malaria huko New York nchini Marekani.
Amesema Tanzania inathamini ushirikiano wa kihistoria uliopo baina yake na Global Fund, mfuko ambao umesaidia kupunguza idadi ya vifo kwa magonjwa ya Ukimwi, Kifua Kikuu na Malaria.
Dkt. Mpango ameishukuru bodi ya Global Fund kwa kuiunga mkono Tanzania kwa miaka mingi pamoja na kuzishukuru na kuzipongeza serikali, mashirika, taasisi na watu binafsi wote kwa michango yao kwa mfuko huo kwa kipindi cha miaka 20 iliyopita.
Makamu wa Rais amesema Tanzania imejitolea kufikia lengo la kimataifa la kukomesha Ukimwi ifikapo mwaka 2030, kwa kutumia teknolojia mpya na mikakati ya kibunifu.
Ameongeza kwamba licha ya mafanikio yaliyopatikana katika kukabiliana na Ukimwi, Kifua Kikuu na Malaria, bado Tanzania inakabiliwa na changamoto ya maambukizi mapya hasa kwa vijana wenye umri wa miaka 15 hadi 24.
Wakati wa mkutano huo, Tanzania imeahidi kuchangia dola milioni moja za kimarekani katika mfuko huo wa kimataifa wa kupambana na Ukimwi, Kifua Kikuu na Malaria, ili kuuwezesha kufanya kazi yake kwa ufanisi.
Baadaye hii leo Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango, anatarajiwa kuhutubia mkutano wa Baraza Kuu la 77 la Umoja wa Mataifa (UNGA), akimwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan.