Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mussa Azzan Zungu, ameitaka wizara ya Fedha na Mipango kuongeza usimamizi wa ukusanyaji wa mapato ya Serikali ambayo ameeleza kuwa hayaridhishi.
Mara baada ya kumalizika kwa kipindi cha maswali na majibu Bungeni jijini Dodoma, Naibu Spika akaitaka serikali kuongeza usimamizi wa makusanyo na kuweka mifumo ambayo itadhibiti upotevu wa mapato.
” Kwa sasa hivi hali ya makusanyo ya serikali hairidhishi na hii inapunguza mapato ya Serikali kwa kiasi kikubwa, mfano makusanyo ya bandari kwa mwezi ni bilioni 95 wakati katika bandari za nchi jirani makusanyo yanafika mpaka bilioni 300 kwa mwezi.” amesema Naibu Spika Zungu
Naibu Spika pia ameitaka wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kuhakikisha inaweka mifumo ya kidijitali itakayowezesha
kampuni za hapa nchini kutoa huduma za intaneti kwa taasisi na ofisi za ndani, badala ya hali ilivyo sasa ambapo fedha nyingi zinalipwa nje ya nchi ili kupata huduma hizo.
“Nakuomba Mheshiwmiwa Nape, wewe ndio mkombozi wa hii nchi kwenye eneo hilo, hebu angalia namna ya kuwawezesha wabunifu wa Tanzania kutoa huduma hizi za intaneti ili kuokoa fedha nyingi ambazo tunalipa kwa watoa huduma hizo nje ya nchi.” amesema Naibu Spika Zungu