Waziri wa Mambo Ndani ya Nchi Kangi Lugola ameliagiza Jeshi la Polisi Nchini kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mawasiliano Nchini (TCRA) kuwabaini na kuwachukulia hatua watu ambao wamekua wakiichafua nchi.
Waziri Lugola ametoa agizo hilo jijini Arusha wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari na kuongeza kuwa serikali haitalifumbua macho suala hilo na kuwataka watu wanaotumia fursa ya kuishi nje ya nchi kuchochea vitendo vya uvunjifu wa amani kuacha mara moja.
Amedai kuwa baadhi ya Watanzania ambao wanaishi nje ya nchi ama wamekwenda katika nchi hizo kufanya shughuli mbalimbali, wamekua wakitumia mitandao ya kijamii kuichafua nchi, jambo ambalo halikubaliki.
Waziri huyo wa Mambo Ndani ya Nchi pia amemtaka Mbunge wa Singida Mshariki, -Tundu Lisu kurejea nchini pamoja na dereva wake ili waweze kutoa ushirikiano kwa vya vyombo vya ulinzi kuhusu tukio la kushambuliwa lililotokea jijini Dodoma Septemba Saba mwaka 2017.
Suala jingine ambalo Waziri Lugola amelitolea agizo ni kukamatwa kwa Mkurugenzi wa Kampuni ya OBC inayomiliki vitalu vya uwindaji katika eneo la Loliondo wilayani Ngorongoro mkoani Arusha, – Isack Mollel kwa madai ya kuwaajiri Raia wa kigeni kufanya kazi bila vibali.
Katika mkutano huo, Waziri Lugola amezungumzia masuala mbalimbali yanayohusu usalama wa nchi na hatua mbalimbali zinazochukuliwa na serikali katika kukabiliana na vitendo vya uhalifu nchini.
Waziri Lugola anaendelea na ziara yake ya kikazi mkoani Arusha, ambapo anatembelea wilaya mbalimbali za mkoa huo pamoja na kuzungumza na watendaji wa taasisi zilizo chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.