Jeshi la Polisi kanda maalum ya Tarime/Rorya, linamtafuta Werema Ibaso mkazi wa kijiji cha Isango wilayani Rorya mkoani Mara kwa tuhuma za kumjeruhi mke wake Maria Marwa.
Ibaso anatuhumiwa kumjeruhi mke wake kwa kumkata mkono na titi, na kumjeruhi vibaya katika maeneo mbalimbali ya mwili hasa kichwani, huku chanzo kikitajwa kuwa ni wivu wa mapenzi.
Kwa mujibu wa mwanamke huyo, baada ya chakula cha jioni mumewe alimuomba simu yake na kumtaka kujaza namba ambazo alikuwa nazo kwenye karatasi ili aone jina lililohifadhiwa katika simu.
Baada ya kugundua namba hiyo haijahifadhiwa kwenye simu ndipo alipoanzisha ugomvi kwa madai kuwa namba hiyo ni ya mwanaume mwingine ambaye amekuwa akiwasiliana naye pasipo yeye kujua.
Maria amedai kuwa baada ya mzozo wa muda mfupi ndipo mume wake alichukua panga na kuanza kumkata ambapo alimkata mkono wa kushoto na titi la kushoto na kisha kumjeruhi maeneo mengine hasa kichwani.
Baada ya kutekeleza ukatili huo, mwanaume huyo alikimbia kusikojulikana huku akimuacha mke wake pasipo na msaada wowote.
Kwa sasa mwanamke huyo amelazwa katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Mara akiendelea kupatiwa matibabu.