Serikali imewahakikishia wadau wote wa sekta ya uvuvi nchini kuwa, ina nia ya dhati ya kuhakikisha kila mmoja ananufaika na sekta hiyo.
Kauli hiyo imetolewa mkoani Dar es Salaam na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wakati wa uzinduzi wa mpango kabambe wa sekta ya uvuvi.
Amesema utekelezaji wa mpango huo kabambe wa sekta ya uvuvi utasaidia kukuza sekta hiyo na kuongeza mchango wake katika pato la Taifa hadi kufikia asilimia 10 kwa mwaka kutoka asilimia 1.8 ya hivi sasa.
Waziri Mkuu amesema kuwa mpango huo ambao utatekelezwa kwa kipindi cha miaka 15 kuanzia 2021/2022 hadi 2036/2037,
una umuhimu mkubwa katika ukuaji wa sekta ya uvuvi pamoja na uchumi wa Buluu.
“Tutaendelea kupokea mapendekezo yenu ili tuweze kuboresha sekta hii, ubunifu wenu ni muhimu, wote tunataka tuzungumze lugha moja.” amesema Waziri Mkuu
Amesema mpango huo unaendana na maono ya Rais Samia Suluhu Hassan katika kuleta mapinduzi makubwa kwenye sekta zote zikiwemo zile za uzalishaji.
“Mpango huu utasaidia kwa kiwango kikubwa kutekeleza dhamira hiyo njema ya Mheshimiwa Rais, tunataka twende kwa kasi zaidi.” amesema Waziri Mkuu Majaliwa