Serikali yatenga bilioni 3 kujenga hospitali Rukwa

0
188

Serikali imetenga shilingi bilioni 3 kwa ajili ya ujenzi wa hospitali ya mkoa wa Rukwa na shilingi milioni 900 kwa ajili ya ukarabati wa majengo yanayotumika katika utoaji wa huduma kwenye hospitali ya sasa.

Naibu waziri Afya Dkt. Godwin Mollel ameliambia Bunge jijini Dodoma kuwa, katika mwaka huu wa fedha serikali imetenga shilingi bilioni 3 kwa ajili ya ujenzi wa hospitali mpya ya mkoa wa Rukwa lakini pia serikali itakarabati majengo yanoyotumika kwa sasa.

Dkt. Mollel ametoa taarifa hiyo wakati akijibu swali la mbunge wa viti maalum mkoa wa Rukwa, Bupe Mwakang’ata aliyetaka kujua ni lini serikali itaanza ujenzi wa hospitali ya mkoa wa Rukwa licha mkoa huo kutenga eneo kwa ajili ya ujenzi huo.

Kuhusiana na uhaba wa madaktari bingwa katika hospitali ya sasa, Dkt. Mollel amesema mpaka kufikia mwezi Oktoba mwaka 2023 madaktari bingwa watatu watahitimu na hivyo watapekwa katika hospitali hiyo.