Serikali imesema inaendelea kupitia mitaala na kupokea maoni kuhusiana na namna ya kuendesha elimu ya shule ya msingi, hasa muda wa masomo kwa wanafunzi wa darasa la saba.
Naibu waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Omar Kipanga amesema, kwa sasa wanafunzi wa darasa la saba wanasoma kwa siku 194 kabla ya kufanya mitihani yao, jambo ambalo wadau wa elimu wamekuwa wakiliona kama halitoi fursa kwa walimu kukamilisha mitaala yao.
Naibu waziri Kipanga alikuwa akijibu maswali ya nyongeza ya Mbunge wa jimbo la Tarime Mjini Mwita Kembaki, aliyetaka kujua ni lini serikali itaruhusu masomo ya ziada “Tuition” kwa wahitimu wa darasa la saba ili kutoa fursa kwa wanafunzi kusoma na kukamilisha mitaala yote katika darasa la saba.
Kipanga amejibu kwa kumweleza Mbunge huyo kuwa kwa sasa wanaendelea kupokea maoni na mapendekezo kwa ajili ya kuboresha mitaala ya elimu, hivyo suala hilo nalo litaangaziwa wakati wa mapitio hayo.