Marais 20 kushuhudia uapisho wa Ruto

0
453

Marais kutoka nchi 20 za Afrika akiwemo Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania, leo wanatarajiwa kushiriki katika sherehe za kuapishwa kwa Rais Mteule wa Kenya, William Ruto.

Sherehe hizo zinazofanyika katika uwanja wa Kasarani jijini Nairobi, pia zinatarajiwa kuhudhuriwa na raia elfu 60 wa Kenya pamoja na viongozi mbalimbali kutoka mashirika ya kimataifa na mabalozi.

Katika sherehe hizo Rais Samia Suluhu Hassan ataongozana na baadhi ya viongozi wa Serikali akiwemo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Balozi Liberata Mulamula, Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara Dkt. Ashatu Kijaji na Harusi Said Suleiman ambaye ni waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

Naibu Rais Mteule wa Kenya, Rigathi Gachagua naye atakula kiapo wakati wa sherehe hizo.

Habari zaidi kutoka nchini Kenya zinaeleza kuwa, Rais Uhuru Kenyatta amekutana na kufanya mazungumzo na Rais Mteule William Ruto hapo jana.

Mazungumzo hayo yamefanyika siku moja kabla ya Ruto kuapishwa, na viongozi hao wamekutana ikiwa imepita miezi kadhaa bila kuwasiliana.