Jeshi la polisi nchini kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama, limewakamata watuhumiwa saba wa matukio ya uchochezi wa migogoro baina ya wakulima na wafugaji katika kitongoji cha Usimbe wilayani Kibiti mkoa wa Pwani.
Kamanda wa Polisi Kikosi cha Kuzuia Wizi wa Mifugo nchini Simon Pasua amesema, watu hao ambao ni wafugaji wanatuhumiwa kuwapiga baadhi ya wakazi wa kitongoji cha Usimbe ambao ni wakulima.
Amesema watuhumiwa hao bado wanashikiliwa na Jeshi la polisi na majina yao yanahifadhiwa kwa sababu za kiupelelezi.
Kwa mujibu wa Kamanda huyo wa Polisi Kikosi cha Kuzuia Wizi wa Mifugo nchini,
watuhumiwa hao wamehojiwa na kukiri kufanya matukio hayo kama iliyoonekana katika picha ya video iliyosambaa katika mitandao ya kijamii.
Watuhumiwa hao watafikishiwa katika vyombo vya sheria pindi upelelezi utakapokamilika.