Mfalme Charles III wa Uingereza amesimikwa rasmi kushika kiti cha ufalme, kufuatia kifo cha Malkia Elizabeth II aliyefariki dunia Alhamisi iliyopita akiwa na umri wa miaka 96.
Sherehe za kusimikwa kwa Mfalme Charles III zimehudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo wa kidini na kisiasa, kama Waziri Mkuu wa Uingereza Liz Truss na mawaziri wakuu wa zamani wa nchi hiyo Tony Blair na Boris Johnson.
Awali kabla ya kusimikwa, mfalme huyo wa Uingereza alilihutubia Taifa kwa mara ya kwanza akiwa Mfalme, na kuahidi kuwahudumia wananchi kwa upendo na uadilifu, pamoja na kuenzi uongozi bora ulioachwa na Malkia Elizabeth II.
Amesema kifo cha Malkia Elizabeth II ni pigo kubwa kwa wananchi wa Uingereza na hata wa mataifa mbalimbali duniani
Wakati hayo yakiendelea, baadhi ya wananchi na viongozi nchini Uingereza na sehemu mbalimbali duniani, wanaendelea kutoa salamu za rambirambi kufuatia msiba huo na kusema, Malkia Elizabeth II atakumbukwa kwa mengi hasa ustawi wa nchi hiyo na wananchi wake pamoja na utangamano na Jumuiya ya Kimataifa.
Malkia Elizabeth II ambaye alizaliwa mwaka 1926, amekuwa malkia wa kwanza kuongoza nchini Uingereza kwa muda mrefu, ambapo ameshika wadhifa huo kwa takribani miaka 70.