Nkamia awapiga msasa watangazaji wa mpira

0
235

Mtangazaji wa zamani wa mpira wa miguu Juma Nkamia amewasihi watangazaji wa mpira wa miguu wa sasa kuendana na mabadiliko ya teknolojia, ili kutopoteza mashabiki na wafuatiliaji wa soka kupitia redio.

Nkamia amesema hayo mkoani Dar es Salaam wakati wa kufunga mafunzo ya siku tatu ya watangazaji wa mpira wa miguu yaliyoandaliwa na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) yenye lengo la kuwakumbusha kuwa na taarifa muhimu za mchezo pamoja na kutangaza kwa umakini.

“Tuepuke baadhi ya mambo ambayo yatamfanya msikilizaji kujiuliza mara mbili mbili kuwa mtangazaji alimaanisha nini, kweli kuna maneno ambayo unaweza kupata wakati mgumu kuyaelezea lakini jengeni utamaduni wa kuyaeleza kwa urahisi ili anayekusikiliza usimpe kazi nyingine ya kujiuliza hapa mtangazaji kamaanisha nini.” amesema Nkamia

Kuhusu kuiga jambo kwa mtangazaji mwingine, Nkamia amesema si vibaya kuiga lakini usiige mpaka mtu ahisi kabisa kuwa wewe unamuiga mtu fulani.

“Kuiga si vibaya ila iga halafu ongeza vya kwako hapo utakuwa bora. Kawaida mtangazaji wa mpira ni mtu wa kujifunza kila siku ili msikilizaji asikuchoke, hivyo ubunifu wako utamfanya mtu akuone mpya kila siku, ukiwa umeona mtangazaji fulani anatangaza vizuri ukahisi kuna vitu vinakufaa chukua halafu ongeza vya kwako.”ameongeza Juma Nkamia

Mafunzo hayo ya siku tatu kwa watangazaji wa mpira wa Shirika la Utangazaji Tanzania, yamejumuisha wadau wa mpira wa miguu nchini wakiwemo Bodi ya Ligi, Waamuzi waandamizi na Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF).