Rais Abdelaziz Bouteflika wa Algeria ametangaza kugombea kiti hicho kwa muhula mwingine wa Tano katika uchaguzi utakaofanyika mwezi Aprili mwaka huu.
Taarifa iliyotolewa kupitia vyombo vya habari vinavyomilikiwa na serikali imemkariri Bouteflika akisema kuwa, bado anahitaji kuwatumikia raia wa Algeria licha ya maradhi yanayomsumbua.
Bouteflika mwenye umri wa miaka 81, amekaa madarani kwa muda wa miaka 20 na amekua akionekana hadharani mara chache tangu mwaka 2013 baada ya kupata maradhi ya kiharusi.
Wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanasema kuwa itakua vigumu kwa Bouteflika kutekeleza majukumu yake ya Urais endapo atachaguliwa tena kutokana na hali yake.
Kwa sasa anatumia kiti cha kusukuma na katika miaka ya hivi karibuni ameshindwa kuhudhuria mikutano kadhaa.
Habari zaidi kutoka nchini Algeria zinasema kuwa, Bouteflika ana nafasi kubwa ya kushinda kiti hicho cha Urais kwa mara nyingine katika uchaguzi huo wa mwezi Aprili.