Vodacom yaleta Teknolojia ya 5G inchini

0
1322

Tanzania imekaribisha mapinduzi ya kidigitali na kuipelekea kuingia katika orodha ya nchi chache Afrika zilizopiga hatua ya kufikia teknolojia ya kasi ya 5G kupitia kampuni ya simu za mkononi ya Vodacom.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye katika hafla ya uzinduzi wa teknolojia ya 5G nchini, hafla iliyofanyika mkoani Dar es Salaam.

Waziri Nape amesema kukua kwa teknolojia na ubunifu kunaifundisha jamii kuwa inaweza kuunda mustakabali bora wa kizazi cha sasa na baadae katika nyanja ya uchumi, kwani serikali imekaribisha mapinduzi ya kidigitali nchini ambayo ni kichocheo cha maendeleo.

Pia ameipongeza kampuni ya simu za mkononi ya Vodacom kwa kuifanya Tanzania kuwa moja ya nchi chache barani Afrika, zenye teknolojia ya kasi ya 5G, huku akizitaja nchi zilizotangulia kuwa ni Botswana, Misri, Ethiopia, Gabon, Kenya, Lesotho, Madagascar, Mauritius, Nigeria, Senegal, Seyshelles, Afrika Kusini, Uganda na Zimbabwe.

Waziri Nape amesema serikali inaunga mkono sekta binafsi na mfumo wa uvumbuzi wa teknolojia ya nchini, akizitaja teknolojia mbalimbali kama teknolojia ya vitu “internet of things” , akili bandia “artificial intelligence “ , teknolojia ya block chain, teknolojia ya 5G, roboti na kompyuta kutoa suluhisho ili kulisaidia Taifa kufikia malengo yake.

Aidha amesema serikali imedhamiria kuendelea kujenga mazingira rafiki kuboresha teknolojia ya mawasiliano nchini, ili kutatua changamoto zilizopo katika jamii.

Teknolojia ya kasi ya 5G imezinduliwa rasmi leo na kuanza kutumika kwa baadhi ya maeneo na baadae kuenezwa kote nchini, na kabla ya hapo ilikuwa ikitumika teknolojia ya kasi ya 4G na 3G.