Chanzo NHIF kulemewa chatajwa

0
130

Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amesema magonjwa yasiyoambukiza, urasimu na kuingizwa kwa wanachama wasio watumishi wa umma ambao asilimia 99 ni wagonjwa katika Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), ni miongoni mwa mambo yaliyochangia kulemewa kwa mfuko huo na kuufanya usitimize majukumu yake ipasavyo.

Waziri Ummy Mwalimu ametoa kauli hiyo jijini Dodoma katika mkutano wake na waandishi wa habari, mkutano uliokuwa na lengo la kutoa ufafanuzi kuhusu huduma na madai ambayo yamekuwa yakitolewa na watu mbalimbali kuhusu kulegalega kwa mfuko huo.

Amesema NHIF ilianzishwa mwaka 2001 kwa ajili ya kuwahudumia watumishi wa umma pekee lakini kutokana na uhitaji wa wananchi wengine kutaka kuingizwa, serikali ilifanya marekebisho na kuingiza watu ambao si watumishi, na hapo ndipo ilikuwa chanzo cha tatizo.

Waziri Ummy Mwalimu amesema wangebakizwa watumishi wa umma pekee kusingekuwa na tatizo, lakini tatizo ni baada ya kuingizwa kwa huduma nyingine kama Toto Afya Card ambapo napo watoto wengi wanaojiunga tayari ni wagonjwa.

Ametaja chanzo kingine cha kulemewa kwa NHIF, ni watumishi wa mfuko huo kujiingiza katika vitendo vya udanganyifu, wakishirikiana na vituo vya kutolea huduma za afya.