Mkuu wa mkoa wa Geita, Martine Shigella amemuagiza kamanda wa polisi wa mkoa huo Henry Mwaibambe, kuwakamata wananchi wanaotuhumiwa kuwajeruhi askari wa maliasili watatu wa shamba la miti Silayo lililopo katika halmashauri ya wilaya ya Chato.
Shigella ametoa agizo hilo wakati akiwajulia hali majeruhi hao waliolazwa katika hospitali ya Waja iliyopo kwenye halmashauri ya Mji Geita .
Amesema hatua ya wananchi kujichukulia sheria mkononi na kujeruhi haikubaliki ndani ya mkoa wa Geita.
Kwa upande wake Mhifadhi Mkuu wa shamba la miti Silayo, Juma Mseti amesema askari hao watatu wa maliasili walijeruhiwa wakiwa katika utekelezaji wa majukumu yao ndani ya hifadhi.
Mganga Mfawidhi wa hospitali ya Waja Dkt. Nehemia Chilave amesema hali za majeruhi hao zinaendelea vizuri, na kuongeza kuwa walifikishwa hospitalini hapo wakiwa na majeraha katika sehemu mbalimbali za miili yao ikiwa ni pamoja na mgongoni, miguuni na mikononi.
Shamba la miti Silayo ni la pili kwa ukubwa nchini likiwa na hekta zaidi ya elfu 69, huku la kwanza kwa ukubwa likiwa ni shamba la miti Sao Hill lenye zaidi ya hekta ya laki moja na thelathini elfu.