Watoto wanne wa familia moja wamefariki dunia na wengine saba kujeruhiwa katika ajali ya moto iliyotokea kwenye kitongoji cha Magiri Juu wilayani Uyui mkoani Tabora.
Ajali hiyo imetokea majira ya usiku, baada ya paa la nyasi la nyumba walimolala kushika moto na kuteketeza nyumba hiyo.
Kamanda wa polisi wa mkoa wa Tabora, Richard Abwao amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa hali ya majeruhi ambao wamelazwa katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Tabora, Kitete ni mbaya na wapo katika chumba cha wagonjwa mahututi.
Amesema watoto waliofariki dunia katika ajili hiyo ya moto wana umri wa kati ya miaka mitano na nane.
Jeshi la polisi mkoani Tabora linamshikilia mtu mmoja kwa tuhuma za kuhusika na tukio hilo, huku uchunguzi zaidi ukiendelea.
Watoto waliofariki dunia katika ajali hiyo ya moto ni Kashindye Machiya(8), Shija Samwel(5), Jeremia Samwel(7) na Dotto Masasi (6).