Serikali kupitia wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum imejipanga kushirikiana na wizara za kisekta na wadau mbalimbali, ili kuboresha huduma katika makazi ya wazee nchini.
Hayo yamebainika wakati wa ziara ya Naibu Makatibu wakuu kutoka wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum,
Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) pamoja na wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara katika makazi ya wazee Fungafunga yaliyopo mkoani Morogoro.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo Naibu Katibu mkuu wa wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Amon Mpanju amesema, Serikali imekuja na mikakati ya kuwekeza miradi mbalimbali ya maendeleo na kuwataka wananchi wanaozunguka maeneo hayo kutoyavamia, ili yabaki kuhudumia wazee.
Aidha Mpanju amewasihi wazee kujitokeza katika zoezi la sensa ya watu na makazi ili kuwa na takwimu sahihi za wazee zitakazoisaidia serikali kuweka mipango na mikakati kwa ajili ya kuwahudumia.
Naye Naibu Katibu Mkuu TAMISEMI (Afya) Dkt. Grace Magembe amesema wazee ni hazina, na kwamba serikali itaendelea kuwatunza na kuwahudumia ili kuhakikisha wanaishi katika amani na utulivu kwa kuwawekea mazingira salama.
Amesena suala la kuwatunza wazee ni la jamii, hivyo jamii iwajibike kuwalea na kuwatunza wazee, na kuona jukumu hilo ni la jamii nzima kwa kushirikiana na wadau.
Kwa upande wake Naibu Katibu mkuu wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara Dkt. Hashir Abdalah amesema kuwa, wizara hiyo itashirikiana na wizara ya Maendeleo ya Jamii ili kuhakikisha maeneo ya makazi hayo yanatumika katika kuanzisha miradi ya kimakakati.
Ameongeza kuwa maeneo yaliyopo katika makazi hayo yanaweza kutumika kwa ajili ya kuwekeza katika miradi mbalimbali ya maendeleo kwa maslahi mapana ya kuwahudumia wazee katika makazi hayo kutokana na mapato ya miradi hiyo.
Ziara hiyo ya Naibu Makatibu wakuu kutoka wizara mbalimbali katika makazi hayo ya Fungafunga pia imejumuisha wadau ambao ni pamoja na wa kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO) na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF).
Kwa sasa makazi ya wazee Fungafunga yanahudumia wazee 21, ambao wanapatiwa huduma muhimu za malazi, chakula, huduma za afya na msaada wa kisaikolojia.