IEBC yawasilisha vielelezo mahakamani

0
113

Tume ya Taifa ya Uchaguzi na Mipaka ya Kenya (IEBC), leo imewasilisha mahakamani vielelezo vya fomu namba 34 ambazo zilitumika kwenye uchaguzi mkuu uliofanyika tarehe tisa mwezi huu nchini humo.

Fomu namba 34A, 34B na 34C zilitumika kwenye uchaguzi huo kwa ajili ya kurekodi matokeo ya urais, ubunge na ugavana wa kila kituo nchini humo.

IEBC imekuwa kwenye mgogoro wa ndani tangu makamishna wanne wakiongozwa na Naibu Mwenyekiti Juliana Cherera kujitoa kuhusika na matokeo yaliyotangazwa tarehe 15 mwezi huu na Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati, ambayo yalimpa ushindi wa Urais William Ruto aliyepata kura milioni 7.1 dhidi ya kura milioni 6.9 alizopata Raila Odinga.

Mara baada ya kutangazwa kwa matokeo hayo, Odinga aliyapinga akidai kulikuwa na ukiukwaji wa taratibu za uchaguzi zilizofanywa na Chebukati huku akiwataka wafuasi wake watulie kwa kuwa watafuata sheria kudai haki.

Odinga amefungua kesi ya kupinga ushindi wa Ruto katika Mahakama ya Juu ya Milimani ambako shauri hilo linaendelea na kama mahakama ikithibitisha kulikuwa na ukiukaji wa taratibu inaweza kufuta matokeo hayo ya urais.

Hii ni mara ya pili kwa Odinga kwenda mahakamani kupinga matokeo ya Urais nchini Kenya, ambapo mwaka 2017 alifanya hivyo na mahakama ilifuta matokeo yaliyompa ushindi Rais Uhuru Kenyatta na kuagiza IEBC iitishe uchaguzi mwingine wa urais.