Mrajisi vyama vya ushirika Tabora matatani

0
144

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Shaka Hamdu Shaka amemuagiza Waziri wa Kilimo Hussein Bashe kumuondoa haraka Mrajisi wa Vyama vya Ushirika mkoa wa Tabora, kwa madai amekuwa chanzo cha kukwamisha jitihada za kuwainua wakulima wa zao la tumbaku na kusaabisha malalamiko kwa wakulima wa mkoa huo.

Shaka ametoa agizo hilo alipokuwa akizungumza na wananchi wa kijiji cha Ufumula wilayani Uyui mkoani Tabora, ambapo akiwa kijijini hapo amepokea malalamiko ya wakulima wa tumbaku na miongoni mwa malalamiko hayo ni ya kuwepo kwa urasimu wa kusajiliwa vyama vya msingi (AMCOS).

Shaka amesema amepokea malalamiko ya Mrajisi wa vyama vya ushirika mkoa wa Tabora, Geophrey Chiliga kuwa na changamoto mbalimbali zinazokwamisha jitihada za wakulima.

“Changamoto za bwana huyu imekuwa donda sugu , tumetoka Kaliua analalamikiiwa, tumetoka Sikonge analalamikiwa, tumetoka Urambo analalamikiwa, leo tuko Uyui watu wanalia na huyu bwana. Urasimu umekuwa mkubwa sana.” amesema Shaka

Amesisitiza watamjulisha Waziri wa Kilimo kwamba Mrajisi huyo hafai kuwa Tabora, na hivyo wampangie majukumu mengine sehemu ambayo hakulimwi tumbaku aende akafanye anavyotaka lakini sio Tabora.