Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema mpaka kufikia tarehe 18 mwezi huu, jumla ya kaya 1,002 zenye watu 5,382 zimejiandikisha kwa hiari kuhama katika eneo la hifadhi ya Ngorongoro na kuelekea kijiji cha Msomera wilayani Handeni mkoa wa Tanga, lililotengwa na serikali kwa ajili ya wakazi hao.
Kati ya kaya hizo, tayari kaya 624 zenye watu 3,323 zimehakikiwa na kufanyiwa uthamini na kati ya kaya hizo, kaya 106 zenye watu 536 zimeshahamia kijiji cha Msomera.
Waziri Mkuu amesema hayo wakati akiziaga kaya 25 zenye watu 115 zinazohama kwa hiari kutoka katika eneo la hifadhi ya Ngorongoro kuelekea kwenye kijiji cha Msomera, zoezi lililofanyika kwenye ofisi za mamlaka ya hifadhi hiyo.
Amesema Rais Samia Suluhu Hassan amepongeza uamuzi wa wananchi hao na kwamba serikali itaendelea kuwekeza katika kuboresha miundombinu ya eneo la Msomera.
“Napenda kumhakikishia Mheshimiwa Rais kwamba tulianza kuratibu, tunaendelea kuratibu na kuhakikisha wote walioamua kuhama wanapata faraja.” amesema Waziri Mkuu
Amesema zoezi la kuratibu uhamaji wa hiari kuelekea Msomera limefanywa kwa utaratibu mzuri ikiwa ni pamoja na kuzingatia mazingira rafiki yaliyoko katika eneo la Msomera kwa binadamu na mifugo.
“Serikali imetoa fedha kujenga miundombinu ya barabara, umeme, maji, shule huduma za afya na huduma nyingine za kijamii ikiwemo uwezo wa umiliki wa ardhi, kilimo na malisho.” amesema Waziri Mkuu Majaliwa