Jeshi la Polisi latakiwa kutenda haki

0
141

Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango amelitaka jeshi la polisi nchini kutenda haki pasipo kuonea mtu yeyote.

Amesisitiza mtu yeyote anayevunja sheria achukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria na si vinginevyo.

Makamu wa Rais ameyasema hayo mkoani Dar es Salaam, alipokutana na kufanya mazungumzo na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Camillus Wambura.

Dkt. Mpango pia amemuagiza IGP Wambura kuangazia malalamiko yanayotolewa na wananchi kwa jeshi la polisi na kuwachukulia hatua askari wachache wanaoharibu taswira ya jeshi hilo.

Katika mazungumzo hayo Makamu wa Rais amelipongeza jeshi la polisi kwa kuendelea kuimarisha amani pamoja na ulinzi wa wananchi na mali zao.

Amesema kazi ya kulinda raia na mali zao ndio msingi wa maendeleo ya nchi, hivyo jeshi la polisi linapaswa kuendelea kuhakikisha utulivu unapatikana wakati wote.

IGP Wambura alifika kwa Makamu wa Rais kwa lengo la kujitambulisha mara baada ya kuteuliwa na kuapishwa na Rais Samia Suluhu Hassan kuwa mkuu wa Jeshi la Polisi nchini.