Rais Samia Suluhu Hassan amesema kuna baadhi ya Maafisa wa Uhamiaji wanaweka mifukoni mwao fedha zinazotolewa kwa ajili ya visa na vibali badala ya kuziingiza kwenye mfumo.
Rais Samia amesema hayo wakati akifunga mafunzo ya awali katika chuo cha uhamiaji kilichopo Boma Kichakamiba mkoani Tanga, na kusema kuwa katika utafiti mdogo uliofanywa mapema mwaka huu hasa vituo vya Zanzibar na Dar es Salaam, kumegundulika upotevu mkubwa wa fedha za visa ambao unafanywa na maafisa uhamiaji.
“Vitendo vya aina hii, viende vikakomeshwe ndani ya jeshi hili, na turudi kwenye maadili ya jeshi kama wimbo wenu mlivyokuwa mkiimba hapa, na wale wote waliohusika na mambo yale washughulikiwe ili kutoa taswira kwamba anayekosea ndani ya jeshi anashughulikiwa na wengine watoto wapya hawa hawatakiwi kuiga vitendo vya kaka zao na Dada zao wanaowakuta”-amesema Rais Samia.
Ameongeza kuwa wakishughulikiwa waliokula pesa za umma, maafisa wapya watajifunza nidhamu ya kazi, na watajua kuwa adhabu zipo ndani ya jeshi na kumsisitiza Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Dkt. Anna Makakala kulisimamia suala hilo.