Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amesema huduma za uchunguzi na matibabu ya kibingwa kwa kutumia CT SCAN zitaanza kutolewa katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Iringa kuanzia Septemba 15 mwaka huu.
Waziri Ummy amesema hayo alipokuwa akizungumza na wananchi wa mkoa wa Iringa kwenye mkutano wa hadhara wa Rais Samia Suluhu Hassan katika uwanja wa Samora mkoani Iringa.
Amesema hakutokuwa na sababu tena kwa wakazi wa Iringa kwenda kwenye mikoa ya Dodoma au Mbeya kufuata huduma za CT SCAN.
Ili kusogeza karibu zaidi huduma za afya kwa wananchi, Waziri Ummy Mwalimu amesema, amepokea ombi kutoka kwa Mbunge wa viti maalum mkoa wa Iringa, Ritha Kabati la kupeleka daktari wa mifupa katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Iringa na ameahidi kupeleka daktari huyo.
“Niko hapa na Rais wangu Mhe. Samia Suluhu Hassan, nataka niwaahidi wana Iringa tutaleta daktari bingwa wa mifupa katika hospitali yetu ya rufaa ya Iringa ili tuwapunguzie safari za kwenda Dodoma au Mbeya kwa ajili ya kupata huduma za daktari bingwa wa mifupa.” amesema Waziri Ummy Mwalimu