UNFPA yahamasisha vijana kushiriki sensa

0
170

Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu (UNFPA) upande wa Tanzania, limewataka vijana nchini kushiriki sensa ya watu na makazi, ili serikali iweze kufahamu idadi ya vijana waliopo nchini pamoja na mahitaji yao

Akizungumza na waandishi wa habari mkoani Dar es Salaam, mwakilishi mkazi wa UNFPA Dkt. Wilfred Ochan amesema, kila kijana napaswa kujua umuhimu wa kuhesabiwa ili kuwa na takwimu sahihi za vijana.

Amesema hatua hiyo itaisadia UNFPA kwa kushirikiana na serikali kuendelea kuwasaidia vijana katika kuwajengea uwezo wa kiuongozi, ujasiliamali pamoja na elimu ya kujitambua.

“Sensa ya Tanzania inaleta data za kina na zilizogawanyika zaidi ya idadi ya watu, zikiwemo takwimu za Idadi ya watu, Kijamii na kiuchumi. Data ya sensa ni muhimu ili kufahamisha ufanyaji maamuzi kuhusu ugawaji wa rasilimali na uundaji wa sera, ikiwa ni pamoja na sera zinazowalenga vijana na upangaji wa programu ambazo sisi pamoja tunazitetea.” ameongeza Dkt. Ochan

Sensa ya watu na makazi itafanyika nchini kote tarehe 23 mwezi huu.

UNFPA Tanzania imefanya mkutano na waandishi wa habari ikiwa ni maandalizi ya siku ya vijana duniani ambayo huadhimishwa kila tarehe 12 ya mwezi Agosti.

Kwa mwaka huu Tanzania itaadhimisha siku hiyo kwa kauli mbiu inayosema kuwa “kila mmoja anahusika kujenga uchumi imara, ustawi na maendeleo endelevu, jiandae kuhesabiwa.”