Mkutano wa CAF wafunguliwa rasmi

0
161

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amefungua mkutano mkuu wa 44 wa Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF) unaofanyika jijini Arusha.

Mkutano huo umehudhuriwa na watu mbalimbali akiwemo Rais wa Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) Gianni Infantino.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mkutano huo Waziri Mkuu Majaliwa amesema, Tanzania inajivunia kuwa miongoni mwa nchi tatu Barani Afrika zenye timu za wanawake wenye umri wa chini ya miaka 17 zinazoliwakilisha bara hilo kwenye michuano ya Kombe la Dunia itakayofanyika mwezi Oktoba mwaka huu nchini India.

Nchi nyingine ni Morocco na Nigeria.

Pia amepongeza uhusiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na CAF pamoja na FIFA, ambao amesema umekuwa chachu katika kuendeleza soka nchini na kwenye ukanda wa Afrika Mashariki.

Waziri Mkuu Majaliwa amewaeleza wajumbe wa mkutano huo mkuu wa 44 wa CAF ambao wanatoka katika nchi 52 Barani Afrika kuwa, Tanzania inaishukuru FIFA kwa uwekezaji kupitia TFF, kwa ujenzi wa vituo viwili vya michezo kwenye miji ya Tanga na Dar es Salaam.