Bwege aitwa kampeni za Odinga

0
161

Aliyewahi kuwa mbunge wa jimbo la Kilwa Kusini mkoani Lindi kupitia Chama Wananchi (CUF), Selemani Bungara maarufu Bwege, amekwenda nchini Kenya kwa lengo la kumpigia kampeni mgombea wa kiti cha Urais nchini humo kupitia muungano wa Azimio la Umoja, Raila Odinga.

Bwege ambaye mwaka 2020 aligombea ubunge katika jimbo la Kilwa Kusini kupitia chama ACT Wazalendo, anakuwa mwanasiasa wa kwanza kutoka Tanzania kupewa heshima na timu ya kampeni ya Azimio la Umoja kumfanyia kampeni mgombea wao wa kiti cha Urais.

Taarifa iliyolewa kwa vyombo vya habari na chama cha ACT Wazalendo imeeleza kuwa, mvuto na hotuba alizokuwa anazitoa Bwege akiwa bungeni ni miongoni mwa sifa zilizomfanya aitwe na timu hiyo ya kampeni ya mgombea Urais wa Kenya kupitia muungano huo wa Azimio la Umoja.

Uchaguzi mkuu nchini Kenya umepangwa kufanyika tarehe 9 mwezi huu, huku mchuano mkali kwa kiti cha Urais ukionekana kati ya Raila Odinga na Naibu Rais wa Kenya, William Ruto kutoka muungano wa Kenya Kwanza.