Mabadiliko yaliyofanywa NHIF yasitishwa

0
232

Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) umesitisha utekelezaji wa mabadiliko yaliyofanyika hivi karibuni katika mfumo wake wa utambuzi na udhibiti wa huduma kwa wanufaika wa mfuko huo kuanzia hii leo.

Mabadiliko hayo ambayo ni katika mfumo wa utoaji huduma na vituo vya kutolea huduma vilivyosajiliwa kutoa huduma kwa wanufaika wa NHIF, yalikuwa na lengo la kuepusha matumizi ya huduma za bima ya afya yasiyo sahihi na hivyo kuongeza gharama zisizo za lazima.

NHIF imesitisha utekelezaji wa mabadiliko hayo baada ya kujitokeza kwa changamoto ambazo zimesababisha usumbufu usiotarajiwa kwa wadau wa mfuko huo katika hatua za awali za utekelezaji wake.

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa NHIF Celestin Muganga imeeleza kuwa, mfuko huo umepokea maoni na ushauri juu ya namna bora ya kutekeleza maboresho hayo na kuanza kuyafanyia kazi bila kuathiri upatikanaji wa huduma kwa wanufaika wake.