Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) imewasilisha bungeni taarifa ya shughuli za kamati kwa mwaka 2018, taarifa inayoonyesha mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na uchambuzi wa taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuhusu uhakiki wa mfuko mkuu wa serikali.
Akiwasilisha taarifa hiyo Mwenyekiti wa PAC, -Naghenjwa Kaboyoka amesema kuwa sababu ya tofauti ya Shilingi Trilioni Moja Nukta Tano katika ripoti ya mwaka ya CAG kwa mwaka 2016/2017 imetokana na kusanyo la Shilingi Trilioni 25.3 na fedha zilizotolewa na hazina Shilingi Trilioni 23.8 kama ilivyoripotiwa na CAG katika ripoti ya hesabu za serikali kuu iliyoishia Juni 30 mwaka 2017.
Kamati hiyo ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali pia imebainisha uwepo wa uwekezaji usiokuwa na tija uliofanywa na Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) katika ununuzi ya ardhi.
Mwenyekiti huyo wa PAC Naghenjwa Kaboyoka ameishauri serikali kuzifanyia kazi kwa wakati hoja za ukaguzi zinazotolewa na CAG.
