Taarifa ya makusanyo ya halmashauri yatolewa

0
115

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Innocent Bashungwa leo ametoa taarifa ya ukusanyaji wa mapato ya ndani na matumizi ya halmashauri kwa kipindi cha robo ya nne ya mwaka wa fedha wa 2021/22 na kuzitangaza halmashauri tano bora kwa ufanisi wa kiutendaji.

“Katika kipindi cha Julai 2021 hadi Juni 2022, tathmini ya ufanisi wa utendaji wa halmashauri ni alama 80 kati ya 100, tathmini hii imezingatia ukusanyaji wa mapato na matumizi ya mapato ya ndani, ujibuji wa hoja na utekelezaji wa mapendekezo ya CAG, utoaji wa mikopo ya asilimia 10, usimamizi na matumizi ya fedha za marejesho pamoja na matumizi ya Tovuti za halmashauri katika kuhabarisha wananchi.” amesema Waziri Bashungwa na kuongeza kuwa

“Muhtasari wa matokeo ya tathmini unaonesha halmashauri 30 zimefanya vizuri kwa kupata alama kati ya 81-100, halmashauri 61 zimepata alama kati ya 75 – 80, halmashauri 84 zimepata alama 61 – 74, na halmashauri 9 zimepata alama kati ya 41-60 na hakuna halmashauri iliyopata chini ya alama 50.”

Aidha Waziri Bashungwa amesema matokeo hayo yanaonesha halmashauri ya Mji wa Mbulu imeongoza kwa kupata alama 89 ikifuatiwa na halmashauri ya wilaya ya Simanjiro alama 88.7, halmashauri ya wilaya ya Karatu alama 87.6, halmashauri ya Mwanga alama 87.4 na halmashauri ya Tunduma alama 87.3.