Jeshi la Polisi latoa tamko ushauri wa Kinana

0
212

Jeshi la Polisi limeanza kufanyia kazi ushauri uliotolewa na Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Kanali Mstaafu Abdulrahman Kinana kuhusu kupunguza askari wa trafiki mjini.

Kupitia taarifa iliyotolewa na Msemaji wa Jeshi la Polisi Tanzania SACP David Misime ameeleza kuwa Jeshi la Polisi limeanza kuufanyia kazi ushauri huo kuanzia leo tarehe 29.07.2022 kwa kuweka mikakati mizuri ya kutekeleza ambao pia umepokelewa kwa maoni mengi kutoka Kwa wananchi.

“Taasisi yeyote hasa inayohudumia jamii moja kwa moja kama Jeshi la Polisi, ili utendaji wake uweze kuboreshwa kila mara na uendane na matarajio ya wananchi na wadau wengine ni lazima kupokea ushauri, maoni na malalamiko na kuyafanyia kazi kwa wakati ili kuboresha utendaji wake na kuwaondolea kero wananchi.” Amesema SACP Misime

Ameongeza kuwa, Jeshi hilo la Polisi lipo wazi kupokea maoni na ushauri kutoka kwa mtu yeyote mwenye lengo la kuboresha kitengo chochote au utendaji wake Jeshi la Polisi kwa ujumla ili huduma nzuri zaidi kwa watanzania iweze kutolewa na kupunguza malalamiko kama sio kuyamaliza kabisa.

Jana Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Tanzania Bara, Kanali Mstaafu Komredi Abdulrahman Kinana alimshauri Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP), Camilius Wambura, kufanya tathimini ili kuona kama inawezekana kupunguza idadi ya askari wa usalama barabarani ambao wamekuwa wakilalamikiwa kusababisha kero kwa wananchi.

Malalamiko hayo ya wananchi yaliendelea kuibuka hata kwenye kikao cha ndani cha Wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Songwe ambapo mmoja wa wanachama wa Chama hicho ambaye ni dereva wa magari ya kubeba abiria maarufu kama Costa, kutoa malalamiko yake mbele ya Kinana akidai wamechoka kusimamishwa mara kwa mara na matrafiki na kila wanaposimama wanatozwa Sh. 2000 kwa kila kituo.