Timu ya Newcastle United ya nchini England imevunja rekodi yake ya usajili kwa kumsajili kiungo mchezeshaji Mparaguay Miguel Almiron kutoka timu ya Ligi Kuu ya Marekani (MLS), -Atlanta United kwa kitita cha Paundi Milioni 20.
Usajili huo umevunja rekodi ya usajili wa Michael Owen ambapo timu hiyo ya ST James Park ilitumia kiasi cha Paundi Milioni 16 mwaka 2005.
Almiron mwenye umri wa miaka 24 alifunga magoli 13 msimu uliopita na kuisaidia Atlanta United kutwaa ubingwa wa Marekani.
Kiungo huyo Mchezeshaji ameshawahi kucheza kwenye timu za Cerro Porteno ya nyumbani kwao Paraguay na Lanus ya Argentina.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kukamilisha usajili huo, Almiron amesema kuwa amefurahi kujiunga na Newcastle United, klabu yenye historia kubwa.
Newcastle United pia imemsajili mlinzi Antonio Barreca kwa mkopo hadi mwishoni mwa msimu kutoka timu ya Monaco ya nchini Ufaransa.