Serikali yasema Homa ya Mgunda isizuie ulaji nyama

0
126

Serikali imesema ugonjwa wa Homa ya Mgunda usiwe kikwazo cha watanzania kutokula nyama na kwamba asilimia tisini ya nyama inayopitia kwenye machinjio rasmi iko salama.

Akizungumza jijini Dodoma kupitia vyombo mbalimbali vya habari, Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Hezron Nonga amesema, nyama ya mnyama anayechinjwa kwenye machinjio rasmi huwa inakaguliwa na mtaalamu wa mifugo wa serikali kabla ya kwenda sokoni ili kuepusha madhara yoyote kwa binadamu.

Prof. Nonga amebainisha kuwa kutokana na utafiti uliofanywa umebaini kuwa mnyama ambaye ameathirika na vimelea vya ugonjwa wa Homa ya Mgunda akitolea mfano wa ng’ombe, nyama yake inakuwa na rangi ya njano hivyo ni rahisi kwa mtaalam wa mifugo kubaini nyama hiyo machinjioni na kutoruhusu kupelekwa sokoni.

Ameongeza kuwa njia nyingine ya watanzania kujikinga na ugonjwa wa Homa ya Mgunda ni kuhakikisha nyama inapikwa vyema na kuiva ili kuua vimelea vya ugonjwa huo ambavyo vinaishi kwenye majimaji ya mnyama ambaye ameathirika, ukiwemo mkojo na kinyesi chake.

Aidha, Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Hezron Nonga amewataka watanzania kutokula nyama ya wanyama wasiyo rasmi kwenye chakula akiwemo panya kwa kuwa amebainika kuwa ni moja ya wanyama ambao wanahusishwa kwa kiasi kikubwa kubeba vimelea vya ugonjwa wa Homa ya Mgunda na magonjwa mengine.