Majeruhi wa ajali Mtwara wahamishiwa Muhimbili

0
152

Majeruhi saba kati ya 15 wa ajali ya gari iliyotokea hapo jana mkoani Mtwara ambao walilazwa katika hospitali ya rufaa ya mkoa Ligula, wamepewa rufaa kwenda hospitali nyingine kwa ajili ya kupatiwa matibabu zaidi.

Katika ajali hiyo watu 13 wakiwemo wanafunzi 11 wa shule ya msingi ya King David walifariki dunia baada ya breki za basi dogo la shule hiyo kufeli na kusababisha basi hilo kuserereka na kutumbukia kwenye korongo lililopo pembeni ya barabara.

Kaimu mganga mfawidhi wa hospitali ya mkoa ya rufaa – Ligula Dkt. Clemence Haule amesema, majeruhi watatu kati ya hao saba wamepelekwa hospitali ya Taifa Muhimbili mkoani Dar es Salaam na wengine wanne wamepelekwa hospitali ya rufaa ya Ndanda.

Amesema walipokea majeruhi 18 ambapo watatu kati yao walifariki dunia wakati wakiendelea kupatiwa matibabu na kubaki majeruhi hao kumi na watano.