Baadhi ya wanafunzi waliomba lifti

0
152

Wanafunzi watano wa shule ya sekondari ya Mikindani iliyopo mkoani Mtwara ni miongoni mwa wanafunzi waliopata ajali katika eneo la Mjimwema, manispaa ya Mtwara, Mikindani hapo jana.

Katika ajali hiyo watu 13 wakiweko wanafunzi 11 wa shule ya msingi ya King David walifariki dunia baada ya breki za basi dogo la shule hiyo kufeli na kusababisha gari hilo kuserereka na kutumbukia kwenye korongo lililopo pembeni ya barabara.

Mwalimu mkuu wa shule ya sekondari ya Mikindani, Jacob Godfrey amesema, wanafunzi hao watano walipewa lifti na dereva wa basi hilo dogo la shule ya msingi ya King David, ambaye naye alifariki dunia katika ajali hiyo.

Amesema wanafunzi wa shule yake walikuwa watano ndani ya basi hilo ambao wote ni wa kike, na wote ni majeruhi.

Aidha amesema wanafunzi hao ni miongoni mwa majeruhi 15 ambao walipelekwa hospitali ya rufaa ya mkoa wa Mtwara, Ligula.

Mmoja kati ya wanafunzi hao watano wa shule ya sekondari ya Mikindani amepewa rufaa kwende hospitali ya Taifa ya Muhimbili iliyopo mkoani Dar es Salaam na wengine wawili wanapelekwa hospitali ya rufaa Ndanda.

Mwalimu Jacob amesema baadhi ya wanafunzi wa shule hiyo wamekuwa wakiomba lifti kwa dereva wa basi hilo la shule na hata kwenye magari mengine ya watu binafsi ili waweze kuwahi shuleni.