Rais Samia Suluhu Hassan ametuma salamu za rambirambi kwa mkuu wa mkoa wa Mtwara Brigedia Jenerali Marco Gaguti kufuatia vifo vya watu 10 vilivyotokea katika ajali ya gari.
Ajali hiyo imetokea leo saa moja asubuhi katika eneo la mteremko la Mjimwema kata ya Magengeni kuelekea Mitengo, Mikindani mkoani humo.
Kwa mujibu wa kaimu kamanda wa polisi wa mkoa wa Mtwara, Nicodemus Katembo, waliopoteza maisha ni watoto 8 (wasichana 5 na wavulana 3) na watu wazima 2 ambao ni dereva na msaidizi wa gari hilo.
Majeruhi ni 19 (wasichana 13 na wavulana 6) ambao wamepelekwa hospitali ya rufaa ya Ligula mkoani Mtwara kwa ajili ya kupatiwa matibabu.
Kamanda Katembo amesema ajali hiyo imehusisha basi dogo la wanafunzi aina ya hiace lenye namba ya usajili T 207 CTS, mali ya shule binafsi ya awali na msingi ya King David iliyopo mkoani humo.
Ajali hiyo imetokana na gari hilo kushindwa kuhimili breki katika mteremko na kupoteza mwelekeo na hivyo kutumbukia kwenye korongo.
Rais Samia amewapa pole majeruhi wa ajali hiyo pamoja na wafiwa wote na kusema anaungana na familia hizo katika kipindi hiki kigumu cha majonzi.
Mwenyezi Mungu azilaze roho za marehemu wote mahali pema peponi, Amina.