Bunge lakanusha kutomjali Lissu kifedha

0
1104

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Job Ndugai amesema kuwa umefika wakati kwa bunge kujibu hoja mbalimbali zinazotolewa na Mbunge wa Singida Mashariki, – Tundu Lissu dhidi ya Ofisi ya Bunge ikiwemo ile ya Bunge kutomjali kifedha tangu aende kwenye matibabu nje ya nchi.


Akitoa ufafanuzi Bungeni jijini Dodoma mara baada ya kipindi cha maswali na majibu, Spika Ndugai amesema kuwa hadi kufikia mwezi Disemba mwaka 2018 Ofisi ya Bunge ilikua imempatia  Mbunge huyo zaidi ya Shilingi Milioni 250.


Spika Ndugai amesema kuwa kati ya fedha hizo, shilingi milioni 207.8 ni stahiki zake mbalimbali na shilingi milioni 43 ni mchango kwa ajili ya matibabu uliotolewa na Wabunge.


Katika hatua nyingine Spika Ndugai amesema kuwa madai ya Mbunge wa Kigoma Mjini, Kabwe Zitto kuwa ukaguzi maalum uliofanywa na Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu Mkuu wa Hesabu za Serikali – CAG umebaini ubadhirifu wa Shilingi Trilioni Moja nukta Tano hayana ukweli wowote.