Ujenzi wa bomba la mafuta washika kasi

0
187

Mradi wa ujenzi wa bomba la Mafuta Ghafi Afrika Mashariki (EACOP) kutoka Hoima, Uganda hadi Chongoleani, Tanga unaendelea kushika kasi, baada ya kukamilika kwa taratibu za awali za mradi huo.

Akizungumza kwenye Kipindi Cha Jambo Tanzania kinachorushwa na TBC, Mratibu wa mradi huo Asiad Mrutu amesema, kwa sasa kinachoendelea ni kulipa fidia kwa wananchi wanaopisha mradi huo na kuandaa vituo vikubwa na vidogo vitakavyotumika kwenye ujenzi.

Amesema mradi huo utapita katika mikoa nane, wilaya 24 huku wananchi wa mkoa wa Kagera pekee wakilipwa takribani shilingi bilioni 7 kama fidia, baada ya kipisha mradi huo ambapo kutajengwa kambi mbili na kituo cha kusukuma mafuta kimoja.

Uganda imegundua mafuta ghafi takribani mapipa bilioni 6.5, huku EACOP ikianza kuzalisha zaidi ya mapipa bilioni moja.

Makadirio ya mapato yatakayopatikana kutokana na mradi huo ni takribani shilingi trilioni 2.3.

Bomba hilo la mafuta ghafi kutoka Hoima, Uganda hadi Chingoleani, Tanga litakuwa na urefu wa kilomita 1,443 ambapo inatarajiwa kuzalisha ajira elfu 10 hadi elfu 15 kwa Watanzania.

Mradi wa ujenzi wa bomba la Mafuta Ghafi Afrika Mashariki ni mradi wa kimkakati wa serikali kupitia Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), unaotarajiwa kutumia miezi 36 hadi kukamilika kwake na unatajwa kuzalisha ajira nyingi kwa Watanzania.

Hadi kukamilika kwake, mradi huo unatarajiwa kugharimu dola bilioni 5.1 za kimarekani.