Mkoa wa Katavi kuungwa gridi ya Taifa

0
155

Makamu wa Rais, Dkt. Philip Mpango ameigiza Wizara ya Nishati kuhakikisha ujenzi wa kituo cha kupoozea umeme wa Gridi ya Taifa cha Inyonga kukamilika ifikapo Oktoba 2023 na mkoa wa Katavi unaunganishwa katika gridi ya Taifa.

Makamu wa Rais amesema alipokuwa akizungumza na viongozi na wananchi wa Wilaya ya Mlele mkoani Katavi mara baada ya kutembelea na kukagua mradi wa ujenzi wa njia kuu ya kusafirisha umeme wa msongo wa Kilovoti 132 kutoka Tabora hadi Katavi katika eneo la Inyonga na kuonesha kutoridhishwa na kasi ya ujenzi wa mradi huo ambao umechelewa kwa takribani miezi nane mpaka sasa.

Katika hatua nyingine ametoa maelekezo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuwataka wakurugenzi kuacha mara moja tabia ya kutoza ushuru kwa mazao yanayosafirishwa chini ya tani moja kwani serikali iliondoa tozo hizo ili kuwasaidia wakulima wadogo kupata kipato. Amesema wakurugenzi wanapaswa kutafuta mbinu sahihi za kuwabaini wanaokusanya mazao zaidi ya tani moja ili kuwanusuru wale wakulima wadogo.

Pia amewaasa wananchi wa Mlele kuendelea kutafuta elimu kuhusu lishe ili wawe na afya bora kulingana na mazao mengi wanayozalisha. Makamu wa Rais amewataka kuendelea na juhudi za kutunza mazingira ikiwemo kupiga vita uchomaji miti na uchafuzi wa mazingira.

Makamu wa Rais amewaagiza wazazi na walezi mkoa wa Katavi kuhakikisha watoto wao wanapata elimu ili taifa kuwa na rasilimali bora zaidi itakayoharakisha maendeleo.

Makamu wa Rais yupo ziarani mkoani Katavi ambapo anakagua miradi mbalimbali ya maendeleo pamoja na kuzungumza na wananchi.