Dkt. Mpango akutana na Balozi Tembele

0
104

Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango leo tarehe 20 Julai 2022 amekutana na kufanya mazungumzo na balozi wa Tanzania nchini Indonesia Macocha Tembele, mazungumzo yaliofanyika Jijini Dar es salaam.

Makamu wa Rais amempongeza Balozi Tembele kwa kuaminiwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwenda kuiwakilisha Tanzania na watu wake katika taifa la Indonesia. Amemuagiza kuhakikisha anakuwa na nyenzo muhimu zinazobeba vipaumbele vya nchi kama vile dira ya maendeleo ya taifa, mpango wa maendeleo wa miaka mitano pamoja na ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya 2020.

Amemuagiza Balozi Tembele kuhakikisha anatekeleza diplomasia ya uchumi kwa kutafuta masoko ya bidhaa zinazozalishwa Tanzania. Aidha amemueleza ni muhimu kutafuta teknolojia rafiki zitakazoweza kusaidia katika kuongeza thamani ya bidhaa zinazozalishwa Tanzania.

Amesema kutokana na nchi ya Indonesia kuwa na uzalishaji mkubwa wa mafuta ya mawese yanayotokana na mchikichi unaopatikana pia Tanzania, hivyo kuimarisha ushirikiano baina ya taasisi za tafiti za kilimo za Indonesia na Tanzania.

Makamu wa Rais amemuagiza Balozi Tembele kuhakikisha anashiriki katika mikutano mbalimbali itakayowezesha kujifunza, kueleza mazuri ya Tanzania pamoja kuvutia wawekezaji. Amesema ni muhimu kuendelea kuitangaza lugha ya Kiswahili katika nchi hiyo ikiwemo kutafuta namna ya lugha hiyo kufundishwa nchini Indonesia.

Amesema ni muhimu kufahamu vema vivutio vya utalii vilivyopo nchini Tanzania ili kwenda kuviuza nchini Indonesia kwa kuwavutia watalii kuja nchini Tanzania.Pia amemuagiza kuwaunganisha watanzania wanaoishi Indonesia ili waweze kuchangia maendeleo ya Tanzania.

Kwa upande wake Balozi Macocha Tembele amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa nafasi aliompa ya kuiwakilisha Tanzania nchini Indonesia pamoja na kutoa shukrani kwa Makamu wa Rais kwa miongozo aliompa na kuahidi kufanya kazi kwa bidii kwa maslahi ya taifa la Tanzania.